ICC yapongeza taarifa kuwa Ntaganda sasa anaelekea The Hague

22 Machi 2013

Mwendesha mashtaka mkuu wa Mahakama ya Kimataifa ya uhalifu, ICC, Fatou Bensouda ameunga mkono taarifa ya kwamba mtuhumiwa wa makosa ya kihalifu huko Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, DRC, Bosco Ntaganda yuko njiani kuelekea makao makuu ya mahakama hiyo mjini The Hague, Uholanzi.

Bi. Bensouda amesema leo ni siku nzuri kwa wahanga wa mzozo wa DRC na pia kwa haki ya kimataifa ambapo amesema wale wanaodai kuteseka kwa muda mrefu mikononi mwa Ntaganda wana matumaini kuhusu hatma yao na kwamba sheria itachukua mkondo wake.

Halikadhalika ameshukuru nchi zote na washirika wa kimataifa na wa kikanda waliowezesha siku ya leo kufikiwa na ametoa shukrani za dhati kwa DRC, Marekani, Rwanda na Uholanzi kwa kufanikisha safari hiyo ya Ntaganda kuelekea ICC.

Hata hivyo amesema bado kuna wengine waliofanya uhalifu dhidi ya kibinadamu ambao hadi sasa hawajulikani waliko akigusia kamanda wa FDLR Sylvestre Mudacumura na viongozi wa juu wa kikundi cha waasi cha Lord’s Resistance Army.