Hali ya usalama Sudan Kusini bado inatia wasiwasi: UNMISS

21 Machi 2013

Mwakilishi wa Umoja wa Mataifa na Mkuu wa Ujumbe wake nchini Sudan Kusini, Hilde Johnson, amesema hatua za kuielekeza nchi hiyo kuwa tulivu na imara ni za mwendo usiolingana kote nchini. Akilihutubia Baraza ka Usalama la Umoja wa Mataifa, Bi Johnson amesema ingawa Sudan Kusini imepiga hatua za maendeleo katika sehemu fulani, bado taifa hilo jipya inakabiliana na changamoto nyingi.

Ameongeza kuwa hali ya uhusuiano kati ya Sudan Kusini na Sudan bado ni tete, ingawa huenda makubaliano ya kutekeleza mkataba wa ushirikiano wa mwezi Septemba 2012, ambayo yalitiwa saini na nchi hizo mbili mnamo Machi 8, 12 na 19 yakasaidia kuimarisha hali katika miezi ijayo.

Amesema kuwa changamoto za usalama wa ndani, hasa ghasia za kikabila, mizozo juu ya ardhi na vitendo vya makundi yenye silaha kwenye majimbo ya Jonglei, Upper Nile na Unity bado ni chanzo cha hali kuyumbayumba, na hatari kwa raia.

Kuzuka kwa machafuko hivi karibuni katika majimbo ya Jonglei na Bahr el-Ghazal kumedhihirisha hata zaidi umuhimu wa jukumu la UNMISS la kuwalinda raia. Hali katika jimbo la Jonglei inazidi kusikitisha, na inatoa changamoto ya kukanganya kwa UNMISS na serikali. Kuongezeka kwa ripoti za kuzuia uhuru wa kujieleza na ukiukwaji wa haki za binadamu katika Sudan Kusini kunatia wasisi.

Bi Johnson pia amesema hali iliyopo Sudan Kusini inaendelea kuwa tishio kwa usalama wa kimataifa, sio tu kwa sababu ya uhusiano wake na Sudan, bali pia kwa sababau kusambazwa kwa silaha kiholela Sudan Kusini kunahatarisha usalama wa nchi tano zingine jirani.