Tuupinge ubaguzi wa rangi michezoni: UM

21 Machi 2013

Ni nini hasa tunachoweza kukifanya ili kuutokomeza ubaguzi wa rangi? Swali hili wameliuliza wataalam wa ngazi ya juu wa haki za binadamu kuhusu ubaguzi wa rangi kwenye Siku ya Kimataifa ya Kutokomeza Ubaguzi wa Rangi, leo Machi 21.

Wataalam hao wamesema siku hii ni muhimu kwa kusherehekea utofauti, na kutoa wito kwa wanamichezo na mamlaka za michezo pamoja na mashabiki kuchukua hatua mathubuti dhidi ya kutovumiliana na ubaguzi wa rangi michezoni.

Akiongea katika jopo la mazungumzo kuhusu ubaguzi wa rangi katika michezo hii leo, Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu, Navi Pillay ametoa wito kwa mamlaka za michezo kukabiliana na ubaguzi wa rangi michezoni kwa njia ya dhati

(PILLAY)

“Ubaguzi wa rangi ni ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu. Ni uhalifu, na ni lazima uchukuliwe hivyo na mamlaka za michezo. Hatua za haraka na za dhati zinatakiwa zichukuliwe ikiwa tunataka kuvitokomeza vitendo vinavyotia dosari sifa ya mchezo wenye unaopendwa zaidi duniani.”

Miongoni mwa wahusika katika jopo hilo, walikuwa wacheza kandanda mashuhuri, Patick Viera na Kevin Prince Boateng, ambaye ameongea kuhusu ubaguzi wa rangi alokumbana nao mwezi Januari mwaka huu, na kutaka hatua mathubuti zichukuliwe

(BOATENG)

“Ni mwaka 2013, na ubaguzi wa rangi bado upo, na ni tatizo sugu. Unapatikana mitaani, maeneo ya kazi na uwanja wa kandanda. Tusipoukabili, utaenea. Ni lazima tukabiliane nao na kuupinga. Hakuna kiwango cha ubaguzi wa rangi kinachoweza kukubaliwa. Haukubaliki, uwe wa aina gani au wapi. Na unapata nguvu kutokana na kuupuuza na kutochukuwa hatua.”

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud