FAO yataka kumalizwa ukataji holela wa misitu

21 Machi 2013

Huku Umoja wa Mataifa ukifanya maadhimisho ya kwanza ya siku ya kimataifa ya misitu, Mkurugenzi mkuu wa Shirika la kilimo na mazao la Umoja wa Mataifa FAO Jose Graziano da Silva amezitaka nchi kuunga mkono lengo la kupunguza hadi sufuri ukataji haramu wa miti.  Amesema kuwa kwenye nchi nyingi ukataji wa miti umeathiri viumbe, umesababisha kuwepo uhaba wa maji masuala ambayo husababisha kutokuwepo usalama wa chakula  hususan kwa watu maskini. Jason Nyakundi na taarifa zaidi.

(SAUTI YA JASON)

Akizungumza kwenye sherehe za kuadhimisha siku ya kimataifa ya misitu hii leo Graziano da Silva amesema kuwa kukomesha ukataji haramu wa miti  na kuzuia upoteaji wa misitu  kutachangia pakubwa  kumaliza njaa, umaskini na kuleta udhabiti. Amezishauri nchi kuunga mkono upanzi wa miti na kuzuia kabisa ukataji haramu wa miti kabla ya mwaka 2015 akiongeza kuwa malengo haya mawili yanastahili kushirikishwa kwa karibu. Mkuu huyo wa FAO amesema kuwa ulimwengu unaweza kupata matokeo mazuri ikiwa mataifa , taasisi za kifedha za kimataifa, Umoja wa Mataifa , mashirika ya umma na yale ya kibinafsi yatashirikiana kutatua masuala haya. Katika hatua nyingine matifa ya Mediterranean yanakutana hii leo nchini Algeria kujadili hali ya misitu ya eneo hilo na kuweka mikakati dhidi ya misitu ya Mediterreanean.

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter