Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Libya na Guinea zamulikwa huko Geneva

Libya na Guinea zamulikwa huko Geneva

Kikao cha baraza la haki za binadamu kinachoendelea Geneva, Uswisi kimepata ripoti za Kamishwa wa tume ya haki za binadamu katika Umoja wa Mataifa kuhusu Libya na Guinea ambapo imesema licha ya kuimarika kwa haki za binadamu bado kuna changamoto.  Akiwasilisha ripoti kuhusu Guniea Naibu Kamishna Mkuu wa haki za binadamu kwenye Umoja wa Mataifa Kyung-Wha Kang amesema nchi hiyo inapaswa kushirikiana  zaidi na mifumo mingine ya haki za binadamu hususan mtaalamu huru wa ukweli na haki, imulike haki za binadamu , malipo ya fidia kwa wahanga na kuepusha dhuluma kurejea. Amegusia pia vurugu za hivi karibuni.

(SAUTI Kwang on Guinea)

“Tangu ripoti hii itolewe tuna wasiwasi wa ongezeko la ghasia zilizoibuka kati ya waandamanaji na majeshi ya ulinzi wakati wa maandamano ya wapinzani tarehe 27 Februari 2013 juu ya uchaguzi ujao wa wabunge. Halikadhalika mapigano kati ya jamii za Peli na mandinke. Tunalaani vikali kitendo cha kushambulia watu na mali kwa misingi ya kabila, na kitendo cha jeshi kutumia nguvu kupita kiasi. Tunaitaka serikali ilinde raia na ihakikishe wahusika wanawajibishwa.”

Kuhusu Libya ripoti hiyo inataja masuala yanayostahili kushughulikiwa kuwa ni pamoja kumaliza vitendo vya watu kushikiliwa vizuizini kutokana na mizozo, kuimarisha utawala wa kisheria na kuwa na mkakati wa kina wa haki na usimamizi wa haki za binadamu. Bi. Kyung-Wha amesema hali nchini Libya imesalia kuwa tete huku ikitarajiwa kufungua ukarasa mpya kwa kuandika katiba mpya.

 (SAUTI  Kwang on Libya)

 

Mamlaka nchini Libya lazima zihakikishe  mchakato wa kupata katiba mpya unakuwa shirikishi na jumuishi kwa lengo la kupitisha  katiba ambayo inalinda hadhi, isiyo ya kibaguzi, yenye usawa na inayotetea haki za binadamu wote.”

=====