Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kuwajali wengine kunajenga furaha: Ban

Kuwajali wengine kunajenga furaha: Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon ametoa salamu zake kwa maadhimisho ya kwanza ya siku  ya furaha duniani hii leo na kusema kuwa bado safari ya kufikia furaha ni ndefu kwa wakazi wengi duniani ambao wamegubikwa na ufukara.  Amesema kwa watu wengi zaidi mizozo ya mara kwa mara ya kiuchumi na kijamii, ghasia, uhalifu, uharibifu wa mazingira na ongezeko ni vitisho vilivyopo wakati wowote dhidi ya furaha kwao. Bwana Ban amesema mkutano wa Rio +20 uliweka bayana umuhimu wa mizania ya maendeleo endelevu inayojumuisha kwa misingi mikuu mitatu ambayo ni ukuaji uchumi, maendeleo ya kijamii na uhifadhi wa mazingira.  Amesema anatiwa moyo kuona baadhi ya serikali zinapima maendeleo kwa kutumia kigezo cha ustawi wa jamii badala ya kutegemea kigezo cha jumla cha pato la ndani la taifa pekee na ametaka nchi nyingine kuiga mfano huo.

Kwa mantiki hiyo Katibu Mkuu amesema katika siku hii ya Furaha duniani, kila mtu aweke upya ahadi ya kujenga maendeleo endelevu kwa kusaidia wengine kwa kuwa kwa kufanya hivyo inawezekana kujenga mustakhbali unaohitajika.