Ajenda ya elimu kwa wote bado kutimia

20 Machi 2013

Zaidi ya wawakilishi 100 wa mashirika ya Umoja wa Mataifa, wahisani, wasomi na mashirika ya kiraia wamekubaliana kuwa mfumo endelevu wa kujiendeleza watoto, vijana na watu wazima uwe kitovu cha ajenda ya maendeleo wakati huu ambapo azma ya elimu kwa wote haijatimia. Wamefikia makubaliano hayo huko Dakar, Senegal kwenye kikao cha kujadili ajenda ya maendeleo wakati huu ambapo utekelezaji wa malengo ya maendeleo ya milenia unafikia ukingoni.

Mmoja wa washiriki, Geeta Rao Gupta ambaye ni Naibu Mkurugenzi Mkuu wa shirika la Umoja wa mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF, amesema watoto wa jamii maskini, walemavu na waishio kwenye maeneo ya migogoro wanashindwa kupata elimu na fursa za kujiendeleza. Amesema licha ya kwamba katika miongo miwili iliyopita fursa ya mtoto kupata elimu imeongezeka kwa watoto zaidi ya Milioni Hamsini kuwepo shuleni, bado watoto Milioni 60 wenye umri wa kuanza shule ya msingi wameshindwa kufanya hivyo.

Amesema ni lazima kuangalia suala la uwiano wakati huu wa maandalizi ya ajenda ya maendeleo baada ya mwaka 2015 ambapo washiriki wameweka mikakati ya kuhakikisha kila mtoto anapata haki yake ya msingi ya kujifunza kwa kuwa elimu siyo tu haki ya msingi bali huwezesha kudai na kupata haki zingine.