Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Graziano Da Silva amwakilisha Ban sherehe za kutawazwa Pope Francis

Graziano Da Silva amwakilisha Ban sherehe za kutawazwa Pope Francis

Mkurugenzi Mkuu wa shirika la chakula na kilimo duniani, FAO, Jose’ Graziano da Silva amehudhuria sherehe za kutawazwa kwa kiongozi wa kanisa katoliki duniani Pope Francis wa I na kusema kuwa Umoja wa Mataifa una matumaini na kiongozi huyo rafiki wa maskini katika kusaidia harakati za kukabiliana na njaa, utapiamlo na ufukara. Graziano da Silva ambaye ameshiriki sherehe hizo akimwakilisha Katibu Mkuu Ban Ki-Moon aliungana na viongozi wengine mashuhuri kwenye umati wa waumini na wageni waliokusanyika viwanja vya kanisa la Mtakatifu Peter huko Vatican, Italia kwa shughuli hiyo.  Mkuu huyo wa FAO amesema kitendo cha Umoja wa mataifa kuunga mkono jitihada za Vatican na madhehebu mengine hakikwepeki katika harakati za kutokomeza njaa, kujenga mustakhbali endelevu na kuboresha maisha ya makundi yaliyo hatarini zaidi.  Amesema jitihada za aina hiyo hazina mantiki kisiasa na kiuchumi pekee, bali pia kimaadili. Graziano da Silva alipata fursa ya kuzungumza na Pope Francis ambapo pia alitoa shukrani kwa mtangulizi wake Benedict wa XVI, kwa mchango wake wa kukabiliana na njaa hususan udhibiti wa ongezeko la bei za vyakula.