Udhibiti wa biashara ya silaha ni muhimu: Ban

15 Machi 2013

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ameunga mkono mpango unaopendekeza kuanzishwa kwa mkataba wa udhibiti wa biashara ya silaha, ikiwa ni wiki moja tu kabla ya kufanyika kwa mkutano wa kimataifa ambao unatazamiwa kuamua juu ya mkataba huo. Nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa zinatazamiwa kukutana wiki ijayo kwa ajili ya kufikia uamuzi kama kupitishwa kwa sheria ya kudhibiti biashara hiyo au la. Katika taarifa yake, Ban ameelezea matumaini yake na anaamini viongozi watakaohudhuria mkutano huo wataweka pembeni tofauti za kisiasa na kuwa na agenda moja ya kupitisha mkataba huo. George Njogopa na taarifa zaidi.

(TAARIFA YA GEORGE)

Mkutano huo juu ya mkataba wa biashara ya sialaha unatazamiwa kuanza hapo Machi 18, Mjini New York na wajumbe wanatazamia kutumia fursa hiyo kuanzisha majadiliano ambayo yatatoa mwangaza namna ya upitishwaji wa mkataba huo. Kwa upande wake, Ban Ki-moon amesema kuwa viongozi wa dunia wanapaswa kuwajibika kwa pamoja na hatimaye kufanikisha shabaha ya udhibiti wa sihala, kuanzia zile ndogo ndogo mpaka kubwa. Amesema kutokana na unyeti wa suala hilo, anaunga mkono hatua ya kuanzishwa kwa mkataba huo na angependelea kuona viongozi hao nao wanachukua mkondo huo huo. Ameeleza kuwa, kuna ulazima wa kuwepo kwa viwango vinavyokubalika kuhusiana na biashara ya silaha hasa wakati huu kunaposhuhudia migogoro ya mara kwa mara .