Ofisi ya Haki za Binadamu yaipongeza serikali ya Kenya kwa uchaguzi wa amani

15 Machi 2013

Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu katika Umoja wa Mataifa (OHCHR), imeipongeza serikali ya Kenya na watu wake kwa kuendesha uchaguzi kwa njia ya amani, na kusema kuwa inatumai Kenya itaendelea kwenye mkondo wa mabadiliko na haki za kijamii.  Timu ya waangalizi wa Ofisi ya Haki za Binadamu waliokwenda Kenya kufuatilia uchaguzi huo wameripoti kuwa uchaguzi ulifanyika kwa njia ya amani na hakukuwa na visa vyovyote vya ukiukwaji wa haki za binadamu katika mfumo wa kuendesha uchaguzi huo. Hata hivyo, wamezingatia baadhi ya changamoto zilizokuwepo, kama vile kuharibika kwa mitambo ya usajili wa wapigaji kura, na watu wengi, hasa walemavu, akina mama waja wazito na wenye watoto wachanga, kushindwa kupiga kura kwa sababu ya muda mrefu wa kusubiri kwenye foleni.