Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tuna wasiwasi na hali ya usalama Bangassou: Vogt

Tuna wasiwasi na hali ya usalama Bangassou: Vogt

Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa huko Jamhuri ya Afrika ya Kati, Margaret Vogt amesema kuwa waasi wa kundi la Seleka wameteka mji muhimu wa Bangassou, kusini mashariki mwa nchi hiyo na sasa Umoja huo hauwezi kufahamu hali ikoje kwa kuwa njia za mawasiliano zimekatwa.  Katika mahojiano maalum na Radio ya Umoja wa Mataifa, Bi. Vogt ambaye pia ni mkuu wa ofisi  ya Umoja huo nchini humo, BINUCA, amesema hali ya usalama nchi nzima si nzuri na kwamba kutekwa kwa mji huo ni mwendelezo wa waasi kushikilia maeneo muhimu wakati huu ambapo wamekuwa wakimshutumu mara kwa mara rais Francois Bozize wa Jamhuri ya Afrika ya Kati kwa madai kuwa anashindwa kutekeleza makubaliano ya amani yaliyotiwa saini kati ya serikali na waasi mwezi Januari mwaka huu.

(SAUTI YA Vogt)

 “Knachofanya Bangassou kuwa muhimu zaidi ni kwa kwamba Bangassou lilikuwa ni lango la kuingilia maeneo ambayo yanadhibitiwa na LRA kwa hiyo hatari na ugumu ambao tunaweza kukabiliana nao katika kufikia raia walioko mji huo ndio vinafanya Bangassou uwe muhimu. Lakini hali ya usalama nchi nzima ni mbaya hivyo tunahitaji kusisitiza umuhimu wa kumaliza huu uasi.”