Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Papa hatarini kutoweka bahari ya Mediteranian na bahari Nyeusi

Papa hatarini kutoweka bahari ya Mediteranian na bahari Nyeusi

Idadi ya papa katika bahari ya Mediteranian na bahari Nyeusi iliyoko kati ya Ulaya Mashariki na bara la Asia imepungua kwa kiasi kikubwa katika karne mbili zilizopita na hivyo kuwa na athari kwa mfumo wa ekolojia ya baharini kwenye maeneo hayo na ule wa ulaji.  Ripoti mpya ya shirika la chakula na kilimo duniani, FAO inaonyesha kuwa kiwango cha uvuaji wa papa kwenye bahari ya Mediteranian imepungua kwa asilimia 97 katika kipindi hicho, jambo ambalo linahatarisha kutoweka kwao iwapo shinikizo la sasa la uvuvi wa viumbe hivyo litaendelea.

Ripoti hiyo inabainisha kuwa licha ya kwamba taarifa si za kutosheleza lakini katika bahari nyeusi, uvuvi wa papa umepungua na kufikia nusu ya kiwango kilichokuwa kinavuliwa mwanzoni mwa miaka ya 1990. Utafiti huo umetaja uvuvi kupindukia wa papa, uvuvi haramu na uharibifu wa mazingira kwenye makazi ya viumbe hivyo kuwa sababu hatarishi za uwepo wao.