UM yasaidia Tume za uchaguzi Tanzania Bara na Zanzibar

13 Machi 2013

Shirika la mpango wa maendeleo la Umoja wa Mataifa, UNDP limetiliana saini na Tume ya Taifa ya Uchaguzi Tanzania, NEC na ile ya Zanzibar ZEC, mradi wa kusaidia kura ya maoni kuhusu Katiba mpya mwaka 2014 pamoja na uchaguzi mkuu mwaka 2015. Chini ya mradi huo wa uwezeshaji wa demokrasia, Umoja wa Mataifa utapatia tume hizo misaada ya kiufundi ambao utaimarisha uwezo wa kitaifa wa kuwa na chaguzi huru, haki na za kuaminika kwa kushirikisha wadau wote kama vile vyama vya siasa, vyombo vya habari na mashirika ya kiraia.

Alberic Kacou ni Mwakilishi Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Tanzania na pia mkuu wa UNDP nchini humo na hapa anafafanua zaidi.

(SAUTI YA Alberic)

“Tutasaidia NEC na ZEC na washirika wengine wa kitaifa kwa miaka mitatu ijayo kwa kuwa sote tunaamini uchaguzi si kitu cha siku moja. Msaada huo utahusisha kura ya maoni kuhusu katiba mwaka 2014 kama ilivyoombwa na NEC. Hii inafuatia uzoefu wetu wa pamoja wa kura ya maoni ya mwaka 2010 ambapo UNDP na washirika ilisaidia kura ya maoni Zanzibar. Pia mradi unahusisha mafunzo ya haki za binadamu na mashauriano kati ya jamii yatakayoweza kusaidia kuhakikisha amani na usalama, jambo ambalo Umoja wa Mataifa linaunga mkono kama ilivyo kwa  watanzania wote.”

Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi nchini Tanzania, Jaji Mstaafu Damian Lubuva amezungumzia msaada huo wa Umoja wa Mataifa.

(SAUTI YA Jaji mstaafu Lubuva)

“Sisi katika Tume ya Taifa Uchaguzi kwanza kabisa ili kuwa na chaguzi za kuaminika ni lazima uboreshe daftari la wapiga kura hiyo ni muhimu sana ili kuhakikisha wale waliofikia umri wa kupiga kura wanakuwa wameandikishwa na kazi hiyo inapaswa ifanyike kwa umakini ili wakati wa kupiga kura wadau mbali mbali wasiwe na pingamizi.”

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter