Twapongeza makubaliano ya Sudan na Sudan Kusini, sasa watekeleze: UM

12 Machi 2013

Siku chache baada ya ripoti kuwa Sudan na Sudan Kusini wametia saini makubaliano yenye lengo la kupatia suluhu la kudumu mgogoro wa mpaka kati yao, hii leo pande mbili hizo zimetiliana saini mbele ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mpango wa utekelezaji wa makubaliano tisa kati yao kuhusu masuala mbali mbali ikiwemo mgogoro wa mpaka.

Akizungumzia hatua hiyo Balozi wa Sudan kwenye Umoja wa Mataifa Daffa-Alla Elhag Ali Osman, amesema hatua hiyo ni ya matumaini na hakuna anayeweza kuzuia utekelezaji wa mpango huo.

(SAUTI YA balozi Sudan)

Hakuna sababu yoyote ile kwa mtu yeyote ndani ya baraza la usalama kuzuia uamuzi wowote wa baraza hilo wa kutia moyo pande zote mbili. Baraza la usalama linapaswa kuendelea kutia moyo pande zote katika kutekeleza makubaliano hayo tisa ambayo tayari wameanza kutekeleza.”

Naye Balozi wa Marekani kwenye Umoja wa Mataifa Susan Rice amesema wajumbe wa baraza wamepongeza utiaji saini na kutaka utekelezaji wa dhati huku baadhi wakionyesha wasiwasi juu ya masuala mengine ambayo bado kupatiwa suluhu.

(SAUTI ya RICE)

Kwa kiasi kimbwa wajumbe walikubali kwamba makubaliano hayo yametiwa saini ni jambo zuri  lakini kikubwa zaidi ni kwamba lazima yatekelezwe la sivyo yatakuwa ni sawa na kipande kingine tu cha karatasi.”