Wakimbizi waliorejea nyumbani Liberia kuwezeshwa: UNIDO

11 Machi 2013

Katika kuhakikisha wakimbizi wa Liberia waliorejea nyumbani wanatangamana vizuri na maisha ya kila siku, Shirika la umoja wa Mataifa la maendeleo ya viwanda, UNIDO limeandaa miradi inayolenga kuwapatia wakimbizi hao mafunzo ya ufundi stadi na ujasiriamali.

Taarifa ya UNIDO imemkariri Mkuu wa kitengo cha teknolojia ya kilimo na viwanda Chakib Jenane akisema kuwa idadi kubwa ya wakimbizi vijana waliorejea nyumbani hawajawai kuifahamu nchi hiyo na hiyo ni changamoto kubwa ambayo wanapaswa kuishughulikia kwani ukosefu wa shughuli za kujipatia kipato unaweza kukwamisha jitihada za utangamano.

Miradi husika ni miwili na kila mmoja una bajeti ya dola Milioni Moja na Nusu kutoka serikali ya Japani ambapo utahusisha pia wakimbizi wa Liberia wenye mpango wa kurejea nyumbani baada ya kumalizika kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe mwaka 2003.

Miradi hiyo itasimamiwa kwa pamoja na tume ya serikali ya usimamizi wa urejeaji wa wakimbzii nchini Liberia.

Kwa wale ambao bado wako Ghana, mradi wa pili chini ya UNIDO utawezesha serikali ya Ghana kuwapatia uwezo wa kushiriki shughuli za kiuchumi kwenye kambi yao ya Buduburam.

Zaidi ya raia laki Saba na Nusu wa Liberia walikimbia nchi yao wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa zaidi ya muongo mmoja.