Ukiukaji wa haki za binadamu Korea Kaskazini umekithiri: Mtaalam wa UM

11 Machi 2013

Mtaalam maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya haki za binadamu nchini Korea Kaskazini (DPRK), Marzuki Darusman, amesema kuna aina tisa tofauti za mienendo ya ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu nchini Korea Kaskazini (DPRK), na ambayo imerekodiwa katika daftari za Umoja wa Mataifa.

Akilihutubia Baraza la Haki za Binadamu mjini Geneva Uswisi, ambako Baraza hilo linafanya kikao chake cha 22, Bwana Dausman amesema mienendo hiyo imeenea, ina uhusiano wa moja kwa moja, na inaonekana kupangwa.

Kwa mujibu wa mtaalam huyo, baadhi ya haki zilizokiukwa ni pamoja na haki ya chakula, mateso na vitendo vya kudhalilisha, vifungo vya kiholela, ubaguzi, haki ya kuishi, haki ya kuwa na usemi pamoja na uhuru wa kutembea. Amesema taarifa za kuaminika zilizopokelewa kuhusu ukiukaji huu zinadhihirisha haja ya uchunguzi wa kina zaidi unaohitajika kufanywa na ofisi ya haki za binadamu.