Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

ICC yatupilia mbali mashtaka dhidi ya Muthaura

ICC yatupilia mbali mashtaka dhidi ya Muthaura

Mwendesha mashtaka mkuu wa Mahakama ya kimataifa ya uhalifu, ICC ya huko The Hague, Fatou Bensouda ametangaza kufuta mashtaka dhidi ya mtuhumiwa wa kesi ya vurugu zilizoibuka nchini Kenya baada ya uchaguzi Mkuu wa mwaka 2007, Francis Muthaura.

Akitangaza uamuzi wake huo hii leo, Bensouda amesema ameuchukuwa kwa uangalifu mkubwa na kwamba ni wajibu wake kuendelea nakesi kama ana amini kuna  uwezekano wa kuwepo kwa mashtaka na kama hakuna ni wajibu wake kufuta. Amesema uamuzi wake umezingatia changamoto ambazo ofisi yake imekumbana nazo kwenye uchunguzi dhidi ya Muthaura.

(SAUTI Bensouda) 

“Suala kwamba watu kadhaa ambao wangetoa ushahidi muhimu kuhusu vitendo vya Muthaura wamekufa, ilhali wengine wana hofu kubwa kutoa ushahidi. Kitendo cha kusikitisha kwamba serikali ya Kenya imeshindwa kuipatia ofisi yangu ushahidi muhimu na kushindwa kutuwezesha kuwafikia mashahidi muhimu ambao wangetupatia mwanga juu ya kesi ya Muthaura. Na tatu kwamba tumeamua kumuondoa shahidi muhimu dhidi ya Muthaura baada ya shahidi huyo kuondoa sehemu muhimu ya ushahidi wake na kukiri kuwa alipokea rushwa.”

Hata hivyo ameeleza bayana hatma ya watuhumiwa wengine katika kesi hiyo.

(SAUTI Bensouda)

 

“Hebu nifafanue jambo moja, uamuzi huu unamhusu Muthaura peke yake, na hauhusu kesi nyingine. Uamuzi wangu wa leo unazingatia masuala mahususi ya kesi dhidi ya Muthauri na si kwa vigezo vingine. Wakati sote tunafahamu yaliyojiri kisiasa nchini Kenya, hayo hayana ushawishi wowote juu ya uamuzi ninaofanya kama Mwendesha mashtaka Mkuu wa ICC. Kama nilivyokuwa nasema kila wakati ICC ni taasisi ya kimahakama.”

  Halikadhalima Bensouda amewapongeza wakenywa kwa kuendeleza amani wakati wa uchaguzi mkuu na wakati huo huo amewakumbusha azma yake ya kuhakikisha kuwa wahanga wa vurugu za mwaka 2007-2008 wanapatiwa haki.