Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tukomeshe aina zote za ukatili dhidi ya wanawake: UN WOMEN

Tukomeshe aina zote za ukatili dhidi ya wanawake: UN WOMEN

Mkuu wa kitengo cha masuala ya wanawake katika Umoja wa Mataifa, Michelle Bachelet, ametoa wito kwa serikali kote duniani zisikubali kuiachia mivutano na hali ya kusita sita kuzuia hatua za kuendeleza hadhi ya wanawake duniani.

Katika ujumbe wake kwenye siku hii ya kimataifa ya Wanawake, (Bi Bachelet amesema wakati siku hii ikiadhimishwa mwaka huu, wawakilishi wa serikali na wanaharakati wanakutana kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York kuhusu kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake. Bi Bachelet amesema ujumbe wake kwa siku ya leo una sehemu mbili: matumaini na uchungu

Amesema ni ujumbe wa matumaini kwa sababu ufahamu na hatua za kuendeleza haki za wanawake vinaongezeka; huku ukiwa ujumbe wa hasira kwa sababu wanawake na wasichana wanaendelea kukumbwa na viwango vya juu vya ubaguzi, ukatili na kutengwa.

(SAUTI YA BACHELET)

“Leo na kila siku tunasema hapana kwa ubaguzi na ukatili kwa wanawake na watoto. Tunasema hapana kwa ukatili wa majumbani na unyanyasaji. Hapana kwa ubakaji na ukatili wa kingono. Hapana kwa biashara haramu ya kusafirisha binadamu na utumwa. Hapana kwa ukeketaji kwa wanawake. Hapana kwa mahari kwa watoto na ndoa za mapema. Hapana kwa mauaji yanayofanywa kwa kisingizio cha hadhi au tamaa. Hapana kwa mauaji ya halaiki kwa wanawake. Hapana kwa dharau. Lakini tunasema Ndiyo kwa amani, haki za binadamu na usawa”