Kumwezesha mwanamke kutanufaisha dunia nzima: IMF

8 Machi 2013

Mkurugenzi Mkuu wa shirika la fedha duniani, IMF, Christine Lagarde amesema kuwa iwapo wanawake watapatiwa fursa ya kutumia kikamilifu vipaji vyao, basi siyo wao tu watakaofaidika, bali ni dunia nzima.Amesema kuwa wanawake wameendelea kukabiliwa na vizingiti vingi, vingine ambavyo baadhi yao vinawanyima uhuru wa kuchagua maisha wayapendayo. Taarifa zaidi na George Njogopa.

(SAUTI YA GEORGE)

Katika ujumbe wake alioutoa wakati wa kuadhimisha siku ya mwanamke duniani,  Bi. Lagarde alizijadilia changamoto zinazoendelea kuwaandama wanawake duniani kote, na kutaja mojawapo kuwa ni ile inayopatikana kwenye mifumo ya ajira.  Katika hilo amesema kuwa, asilimia kubwa ya wanawake wananyimwa fursa ya kupata ajira na hata wale wachache wanaoajiriwa, wengi hao hupata ujira mdogo.  Alitaja baadhi ya mambo ambayo yanawabinya wanawake kukosa fursa ya kusaka ajira zifaazo. Mambo hayo ni pamoja na sheria zinazowakandamiza wanawake, kuwepo kwa mifumo dume, na mifumo ya maisha ambayo inawaweka wanawake kwenye madaraja ya chini.  Hata hivyo Bi Lagarde alisema kuwa IMF itaendelea kuwa na majadiliano ya mataifa duniani ili kuwezesha ustawi bora kwa wanawake na kusukuma mbele agenda ya maendeleo endelevu.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter