Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ndoa za watoto zaidi ya milioni 140 kufanyika kati ya 2010 na 2020: UNFPA

Ndoa za watoto zaidi ya milioni 140 kufanyika kati ya 2010 na 2020: UNFPA

Kati ya mwaka 2011 na 2020, zaidi ya watoto milioni 140 wataingizwa kwenye ndoa za watoto, kwa mujibu wa Mfuko wa Umoja wa Mataifa unaohusika na idadi ya watu, UNFPA.

Kwa mujibu wa taarifa ilotolewa na UNFPA, pamoja na Shirika la Kuhudumia Watoto la UNICEF na Shirika la Afya Duniani, WHO, ikiwa viwango vya sasa vya ndoa za watoto vitaendelea, basi watoto milioni 14 kila mwaka, au 39,000 kila siku wataolewa wakiwa wadogo mno.

Halikadhalika, UNPFA imeongeza kuwa kwa watoto hao milioni 140 watakaoolewa wakiwa chini ya umri wa miaka 18, milioni 50 kati yao watakuwa chini ya miaka 15.

UNFPA imeongeza kuwa licha ya madhara yanayotendeka kwa wasichana hawa wadogo na ubaguzi dhidi yao, hatua chache sana zimechukuliwa ili kuitokomeza desturi ya ndoa za watoto, huku Mkurugenzi Mkuu wa mfuko huo, Babatunde Osotimehin, amesema ni lazima kuwepo ari ya pamoja kuitokomeza desturi hiyo.