Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wakimbizi wa Mali huko Niger waendelea na elimu ya msingi

Wakimbizi wa Mali huko Niger waendelea na elimu ya msingi

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF pamoja na washirika wake limewezesha zaidi ya wakimbizi watoto Elfu Nne Mia Saba wa Mali walioko nchini Niger kuendelea na elimu ya msingi kwenye kambi mbali mbali nchini humo wakati huu ambapo Mali iko katika mgogoro.  Chini ya ushirikiano huo, vifaa vya shule pamoja na mahema Kumi na Moja yametengenezwa na kuwa madarasa kwa wattoto hao ambapo miongoni mwa shule hizo ni ile iliyoko kambi ya Mangaize, kaskazini mwa Niger, inayohudumia watoto Mia Nane na wengine wakitarajiwa kuongezeka siku hadi siku.

Naibu Rais wa kamati ya kambi hiyo ya wakimbizi Bonjoly Aklinine amezungumzia shule hiyo iliyoanza kutoa elimu miezi mitano iliyopita ndani ya nchi  ya Niger inayohifadhi wakimbizi takribani Elfu Hamsini wa Mali.

(SAUTI YA Aklinine)

"Hawa watoto wanaenda shule kwa sababu elimu ndio msingi wa maisha yao ya baadaye. Na watoto hawa ndio taifa la kesho.”

Aboud Zeid ambaye ni Afisa kutoka Plan International, mshirika wa UNICEF katika mpango huo amesema pamoja na elimu watoto wanapatiwa mafunzo yanayowawezesha kutosahau kule walikotoka.

(SAUTI YA Zeid)

"Hii inasaidia watoto kuendelea kuwa na uhusiano na utamaduni wao ili wasisahau walikotoka hata kama wameondoka kwao, kuhakikisha mawazo yale yale yanabakia.”