Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

AMISOM yaongezewa muda hadi mwakani

AMISOM yaongezewa muda hadi mwakani

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, leo kwa kauli moja limepitisha mswada wa azimio nambari 2093, ambalo linaongeza muda wa kuhudumu wa vikosi vya Muungano wa Afrika nchini Somalia, AMISOM, hadi Februari 28 mwaka 2014.

Pamoja na hayo, azimio hilo pia linaiondolea nchi hiyo ya Pembe ya Afrika vikwazo vya silaha za kijeshi.

Akiongea baada ya kura kuhusu azimio hilo, mwakilishi wa Guatemala kwenye Umoja wa Mataifa amesema anaamini azimio hilo linaashiria njia taratibu ya kuimarisha mifumo ya Umoja wa Mataifa nchini Somalia, na kutambua ufanisi muhimu uliofikiwa katika kuweka amani nchini humo, ukiwemo mji mkuu wa Mogadishu.

Hata hivyo, amesema Baraza hilo lisingepitisha kifungu cha kuondolea Somalia vikwazo vya silaha za kijeshi. Kwa upande wake, mwakilishi wa argentina ameunga hilo mkono, akisema kichaohitajika, ni udhibiti mzuri wa silaha hizo kwa serikali ya Somalia, ambayo huenda ikazihitaji kwa sababu za kiusalama na kupambana na uharamia.