Mamilioni wakabikliwa na tishio la njaa Kusini mwa Afrika

4 Machi 2013

Zaidi ya watu Milioni sita Kusini mwa Bara la Afrika wanakabiliwa na njaa kali kutokana na upungufu wa chakula huku wengine wakikabiliwa na magonjwa mbalimbali ikiwemo utapiamlo.

 Kwa mujibu wa shirikisho la kimataifa la Msalaba mwekundu Mpevu mwekundu, tishio hilo ambalo halijapewa umuhimu katika vyombo vya habari kimataifa linazikabili nchi za Angola, Zimbabwe, Lesotho, na Malawi ambapo mafuriko na ukame unatajwa kama sababu ya tishio la njaa na magonjwa mbalimbali hususani utapiamlo.

 Shirikisho hilo limebainisha kwamba Malawi, Angola, Zimbabwe na Leasotho zimeathirika zaidi ambapo nchini Malawi pekee karibu watu milioni mbili wako katika tishio la njaa, nchini Angola zaidi ya milioni moja na laki nane, huku  Zimbabwe ikifuatia kwa kuwa na watu milioni moja na laki sita walio katika tishio la njaa na magonjwa.

 Tayari mpango wa  msaada wa dharura kwa nchi hizo umeshazinduliwa licha ya kwamba Zimbabwe, Lesotho na Angola hazijapewa msaada wa kutosha.

 Mwakilishi wa Shirika la misaada ya kibinadamu la Umoja wa mataifa nchini Afrika Kusini amesema ukanda huo unahitaji msaada wa nguvu ya pamoja kati ya seriakali, mashirika ya  kimaendeleo na kimisaada na wafanyabisahra ili kuzikomboa nchi hizo na kuimarisah uchumi wake.