Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban kutoa mkakati wa mtazamo wake wa maendeleo baada ya 2015

Ban kutoa mkakati wa mtazamo wake wa maendeleo baada ya 2015

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, amesema mnamo mwezi Septemba kwenye hafla maalum, atawasilisha mkakati wa kina kuhusu mtazamo wa maendeleo baada ya mwaka 2015, ambayo ndiyo tarehe ya mwisho ya kufikia malengo ya maendeleo ya milenia. Hafla hiyo ya mwezi Septemba itahusu ukaguzi wa hatua zilizopigwa katika kuyafikia malengo ya milenia, na kutambua mapengo ambayo hayajazibwa, pamoja na changamoto zilizopo.

Bwana Ban ameliambia jopo la ngazi ya juu kuhusu Haki za Binadamu ya kwamba mwongozo wake utatokana na kazi ya Jopo lake la Watu Mashuhuri linalohusika na ajenda ya maendeleo baada ya mwaka 2015, ambalo litatoa ripoti yake mnamo mwezi Mei. Bwana Ban amesema haki ya kupata elimu ni sehemu muhimu ya mtazamo wake.

(SAUTI YA BAN)

"Mara nyingi watu wanaohitaji haki zao zaidi, ndio wasiojua ni nini haki zao. Licha ya kupiga hatua, watoto wengi sana wa shule za msingi bado hawakwendi shule. Wengi wengine huacha shule kabla ya kuiga stadi za kimsingi. Hii ndiyo maana nilizindua Mkakati wa Kimataifa wa Elimu Kwanza. Elimu, huduma za afya, makazi na utoaji wa haki si vitu vya watu wachache kufurahia, bali ni haki kwa wote”

Bwana Ban amesema Haki za BInadamu ni sehemu ya chembe chembe za uhai wa Umoja wa Mataifa, na haki ya kila mtu anapozaliwa.