Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNAIDS na UNDP zaunga mkono pendekezo la kusaidia nchi maskini kuendeleza na kuongeza ugawaji wa dawa muhimu

UNAIDS na UNDP zaunga mkono pendekezo la kusaidia nchi maskini kuendeleza na kuongeza ugawaji wa dawa muhimu

Shirika linalohusika na masuala ya HIV na UKIMWI, UNAIDS na Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa, UNDP, leo yamezindua chapisho jipya linaosema kwamba kushindwa kupanua kipindi cha mpito kwa nchi maskini ili ziweze kuhitimu matakwa ya mkataba kuhusu masuala ya kibiashara yanayohusiana na haki miliki (TRIPS), huenda kukazuia uwezo wa watu kupata dawa za kupunguza makali ya HIV na dawa zingine muhimu kwa watu ambao wanazihitaji zaidi.

Nchi maskini zaidi ndizo zenye watu walio hatarini zaidi duniani, na hubeba mzigo mkubwa zaidi wa afya. Mnamo mwaka 2011, watu milioni 9.7 kati ya watu milioni 34 wanaoishi na virusi vya HIV kote duniani walipatikana katika nchi maskini. Kati yao, watu milioni 4.6 walifuzu kuanza matibabu ya kupunguza makali na dawa za ARV, lakini ni watu milioni 2.5 tu ndio walikuwa wanapata dawa hizo.

Katika nchi 49 ambazo zinaainishwa kama nchi maskini na Umoja wa Mataifa, mzigo wa magonjwa yasiyo ya kuambukiza nao pia unaongezeka. Akiongea wakati wa uzinduzi huo, Msimamizi wa UNDP, Helen Clark, amesema ili nchi hizi maskini kuweza kufikia malengo ya maendeleo ya milenia, upatikanaji wa dawa za ARV na dawa zingine muhimu ni muhimu.

UNAIDS na UNDP zimetoa wito kwa Shirika la Biashara Duniani, WTO kuyazingatia kwa dharura mahitaji muhimu ya nchi maskini kwa sababu ya maendeleo yazo kijamii na kichumi.