Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mzozo wa Mali umesambaratisha elimu na riziki za watu: OCHA

Mzozo wa Mali umesambaratisha elimu na riziki za watu: OCHA

Mkuu wa operesheni za Afisi ya Kuratibu Misaada ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa (OCHA) Bwana John Ging, amesema kuwa madhara ya mzozo wa Mali ni makubwa mno, mzozo huo ukiwa umeathiri shughuli zote za maisha.  .

Bwana Ging amewaambia waandishi wa habari mjini New York kuwa katika ziara yake nchini Mali, watu wengi wamesema wanahitaji kusaidiwa, hasa katika sekta ya kilimo, ili kukarabati sekta hiyo na kuwezesha tena shughuli zao za kutafuta riziki, huku wakihitaji pia msaada wa chakula mara moja.

Akiorodhesha matatizo wanayokumbana nayo watu waloathiriwa na mzozo wa Mali, Bwana Ging amesema, watu wengi wamesema mzozo umeathiri kilimo, uwepo wa nguvu za umeme, mifumo ya huduma za afya, huku wengi zaidi wakitaja suala la elimu kama lililoathiriwa zaidi

(SAUTI YA GING)

“Idadi zinajisemea zenyewe, kwani takriban watoto laki saba wameathiriwa na mzozo, na kuna wengine laki mbili ambao hawapati elimu yoyote kabisa tangu Januari 2012. Idadi ni kubwa, athari pia ni imekithiri. Kukwamuwa sekta ya elimu ni jambo la dharura ambalo linahitaji kuzingatiwa na kila mmoja.”

Bwana Ging amesema isisahauliwe pia kuwa Mali ni sehemu ya eneo la Sahel, ambalo limeathiriwa na ukame na uhaba wa chakula, ikiwa na watu laki tano na nusu wanaohitaji msaada wa chakula kwa dharura, huku wengine milioni moja kaskazini wakiwa hawana usalama wa chakula, na watoto laki sita na nusu wakikabiliwa na hatari ya utapia mlo.