Ban asifu makubaliano ya utaratibu wa kutafuta amani na usalama DRC

24 Februari 2013

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, amesifu hatua ya nchi kumi na moja za eneo la Maziwa Makuu kutia saini makubaliano ya utaratibu wa amani, usalama na ushirikiano kwa ajili ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo na eneo zima.

Akizungumza mjini Addis Ababa, Ethiopia, ambako makubaliano hayo yamesainiwa, Bwana Ban amesema anatumai kuwa mkataba huo utakaribisha nyakati za amani na utulivu kwa watu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na eneo la Maziwa Makuu kwa ujumla, akiongeza kuwa amesikitishwa sana na mateso ambayo raia wamepitia tangu kuzuka machafuko mwezi Aprili mwaka uliopita.Bwana Ban amewashukuru wadau wote kwa mchango wao katika kutafuta suluhu kwa mzozo wa DRC.

Mkataba huo wa utaratibu unataja ahadi na njia za kufuatilia utekelezaji wa makubaliano hayo katika kutatua masuala muhimu ya kitaifa na eneo zima. Bwana Ban amesema ili kuwezesha hilo, njia hizi za kufuatilia utekelezaji zitahitaji uungwaji mkono wa ngazi ya juu kisiasa na kidiplomasia, akiahidi kuwa Umoja wa Mataifa utaendelea kuwa karibu kusaidia utekelezaji wa makubaliano hayo ya Addis Ababa.

“Hafla hii ya kutia saini makubaliano yenyewe ni tukio muhimu. Lakini ni mwanzo tu wa mtazamo wa kina ambao utahitaji uungwaji mkono endelevu. Wadau wa kitaifa na eneo wanahitaji uungwaji mkono wa jamii ya kimataifa. Natoa wito kwa mchango wenu endelevu kisiasa, kitaaluma na kifedha, katika kutekeleza makubaliano haya.

Hali katika mashariki mwa DRC ni lazima ibaki suala la kipaumbele katika ajenda ya kimataifa.”

Bwana Ban ameahidi kumteua mwakilishi maalum ambaye atasaidia katika utekelezaji wa makubaliano hayo, na katika kuweka viwango wastani vya kupima utekelezaji huo unavyoendelea kwenye ngazi ya kitaifa na kieneo. Ameongeza kuwa atatoa ripoti yake maalum kuhusu Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo katika siku chache zijazo, ambayo itataja mapendekezo yake ya njia za kina za kukabiliana na vianzo vya migogoro katika nchi hiyo, pamoja na kuongeza nguvu majukumu ya ujumbe wa Umoja wa Mataifa katika DRC, MONUSCO

Bwana Ban pia amekutana na kufanya mazungumzo moja kwa moja na viongozi kutoka nchi za Maziwa Makuu, wakiwemo Rais Joseph Kabila na Makamu wa rais wa Uganda, Edward Kiwanuka Ssekandi,; Waziri Mkuu wa Ethiopia, Hailemariam Dessaleg Mwenyekiti wa Tume ya Muungano wa Afrika, AU, Dr. Nkosazana Dlamini-Zuma, Waziri wa Mammbo ya Nje wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, Kanali Parfait Anicet Mbay, na Rais wa Musumbiji, Bwana Armando Emílio Guebuza, ambaye pia ni mwenyekiti wa jumuiya ya maendeleo ya Kusini mwa Afrika, SADC.