Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hollywood yamulika mradi wa ILO, yenyewe yatoa angalizo

Hollywood yamulika mradi wa ILO, yenyewe yatoa angalizo

Mamia ya watu mashuhuri katika fani ya uigizaji na utunzi wa filamu wameshiriki katika tukio maalum la kutia shime mradi wa shirika la kazi duniani, ILO unaohusu ajira zinazozingatia uhifadhi wa mazingira. Shughuli hiyo iliyofanyika huko Hollywood, iliratibiwa na mtunzi wa filamu Hans Zimmer na mwongozaji filamu Ron Howard ambapo waliangalia miradi kama ule wa ILO unaotekelezwa nchini Kenya ambapo wanawake vijana wanapatiwa mikopo kuweza kuuza taa za kandili zinazotumia nishati ya jua kwa wanawake wa vijijini ili waache kutumia mafuta ya taa yanayoharibu mazingira na afya.  Zimmer alieleza kuwa mradi huo ni wa aina yake na kuipongeza ILO kwa kubadilisha maisha ya watu wengi hususan vijijini ambako taa hizo zinatumika. Kwa upande wake Mratibu wa kitaifa wa mradi wa vijana wajasiriamali kwa ILO nchini Kenya, George Waigi amepongeza uhamasishaji huo lakini akatoa angalizo.

(SAUTI YA GEORGE-ILO)

Kile ambacho hatutaki kusikia ni mashirika ya misaada kutoa bure taa hizo bila kuangalia muendelezo wake. Lakini ukiwe fursa kwa wanawake kufanya biashara kwa kuuza, kutunza na kuhamasisha matumizi ya kandili zinazotumia nishati ya jua, itakuwa ni kitu cha kudumu. Kwa hiyo hata Hollywood au ILO wakijiondoa mfumo huo unaendelea, watu wanaweza kuendelea kununua, wafanyabiashara wanaweza kuendelea kuhamasisha na watu wengi zaidi wanaweza kupata huduma hiyo.