Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mwaka wa kimataifa wa zao la Quinoa wazinduliwa, Ban atoa angalizo

Mwaka wa kimataifa wa zao la Quinoa wazinduliwa, Ban atoa angalizo

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon amezungumza katika shughuli maalum ya uzinduzi wa mwaka wa kimataifa wa zao la Quinoa [Keen-wa] na kusema kuwa kutambulika kwa zao hilo kutasaidia kuharakisha utimizaji wa malengo ya maendeleo ya Milenia ikiwemo lile la kupunguza njaa kwa asilimia 50 ifikapo mwaka 2015.

Katika hotuba yake Bwana Ban amesema wakulima wa Quinoa wananufaika siyo tu kwa mlo ulio salama ambao wameuzoa kwa miaka mingi, bali pia kwa manufaa ya kipato yatokanayo na mauzo ya zao hilo nje ya nchi.

Amesema ni matumaini yake kuwa mwaka huu wa kimataifa wa Quinoa utachochea matumizi ya zao hilo duniani kote kama mlo na kusaidia uhakika wa chakula, kupunguza umaskini hususan kwa wakulima wadogo na wakati huo huo kuwa na kilimo endelevu. Ametolea mfano zao hilo limeenea nchi za Kenya, Afrika Kaskazini na China.

Hata hivyo Katibu Mkuu ameelezea wasiwasi wake juu ya uwezekano wa wakulima wadogo kuenguliwa kwenye manufaa ya zao hilo wakati huu ambapo linapata umaarufu wa kimataifa.

(SAUTI BAN)

Baadhi ya wakulima maskini wa maeneo  ya Andes wamenufaika na ongezeko la bei na kuongezeka umaarufu wa zao hilo kwenye masoko  ya kimataifa. Lakini ni vyema tukatambua pia hasara zake. Kadri bei zinavyopanda na mahitaji yanaongezeka, kuna hatari kwa wakulima wadogo kuenguliwa kwa kushindwa kupata kwenye masoko yao chakula hiki walichozoea na badala yake wakapata aina nyingine ya chakula cha bei rahisi kilichofungashwa lakini hakina  lishe bora. Hata wakulima wanaweza kushawishika kuuza zao hilo na kula vyakula visivyo na afya.”