Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban na Netanyahu wazungumzia hali ya Mashariki ya Kati

Ban na Netanyahu wazungumzia hali ya Mashariki ya Kati

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Kin Moon amempongeza Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kufuatia ushindi alioupata katika uchaguzi uliofanyika hivi karibuni nchini humo.

Katika mazungumzo yao yaliyofanyika kwa njia ya simu viongozi hao pia wamejadili umuhimu wa kufufua mazungumzo ya amani kati ya Israel na Palestina na hali ya amani katika ukanda huo hususan athari za mgogoro unaoendelea nchini Syria na hofu ya usalama wa Israeli kwa ujumla kutokana na mazingira hayo.

Halikadhalika Bwana Ban amesisitiza juhudi za makusudi zichukuliwe ili Israel na Palestina kushiriki kwa dhati katika mazungumzo ya amani huku akiitaka jumuiya za kimataifa kuunga mkono juhudu za upatikanaji wa amani.

Katibu Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa katika mazungumzo hayo amegusia suala la hali za wafungwa wa Kipalestina wanaoshikiliwa nchini Israel na kutaka hatua za haraka zichukuliwe dhidi ya wafungwa hao ambao wako katika hali mbaya kutokana na mgomo wa kula.