Syria haitaki misaada iingie kupitia mpaka wake na Uturuki: Amos

19 Februari 2013

Umoja wa Mataifa umesema mgao wa hivi karibuni wa misaada ya kibinadamu kwa wakimbizi wa ndani nchini Syria haukuweza kuwafikia wale wote wanaohitaji kutokana na mapigano yanayoendelea nchini humo.

Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa linaloratibu misaada ya kibinadamu, OCHA, Bi. Valeri Amos ametoa kauli hiyo alipozungumza na waandishi wa habari baada ya mkutano wa saba kuhusu usaidizi wa kibinadamu kwa Syria uliofanyika Geneva, Uswisi.

Bi Amos amesema licha ya kwamba wafanyakazi wa misaada wanavuka maeneo ya hatari wakijitahidi kugawa misaada, bado wanashindwa kuwafikia wengi zaidi hususan maeneo ya Kaskazini ambako pengine wanaweza kufikiwa kwa njia mbadala.

Pamoja na kuzorota kwa usalama, Mkuu huyo wa OCHA amegusia tamko la serikali ya Syria la kuzuia misaada ya kibinadamu kupitia mpaka na Uturuki.

(SAUTI YA AMOS)

 

“Serikali ya Syria imeeleza wazi kuwa haitakubali shehena yoyote ile inayoingia nchini humo kutokea Uturuki. Kwa hiyo bila azimio lingine ya Baraza la uaslama, Umoja wa Mataifa na washirika wake hawawezi kuvuka mpaka huo. Na ndio maana tumejikita zaidi kwenye kuvuka maeneo ya mapigano na kuweza kuwasilisha misada kweney maeneo yanayodhibitiwa na Serikali na waasi ndani ya Syria.”

Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa watu Milioni Nne wanahitaji msaada wa kibinadamu nchini Syria ambapo nusu yao ni wakimbizi wa ndani

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter