Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Msimu wa upanzi Mali wakaribia wakulima hawapo: FAO

Msimu wa upanzi Mali wakaribia wakulima hawapo: FAO

Shirika la chakula na kilimo duniani, FAO limesema msimu wa upanzi unakaribia huko Mali lakini kuna wasiwasi kutokana na jinsi ya kurejesha wakulima kwenye maeneo yao baada ya kukimbia mapigano yaliyoanzia kaskazini mwa nchi hiyo.

Hali hiyo ndiyo ilimsukuma Mkurugenzi wa Shirika la mpango wa chakula na kilimo FAO José Graziano da Silva kuwa na mazungumzo na Waziri wa Kilimo wa Mali Baba Bether ambapo inakadiriwa kuwa zaidi ya watu milioni 2 katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi wanakabiliwa na ukosefu wa chakula na nusu ya hao wapo Kaskazini ambako ndiko kwenye hali mbaya ya usalama.

Katika mazungumzo yao wamekubaliana umuhimu wa jumuiya za kimataifa kushirikiana na serikali ya Mali kuwaunga mkono wakulima kurejea kwenye ardhi zao ili kuendelea na shughuli za kilimo.

Zaidi ya watu 400,000 inasemekana wameyakimbia maeneo yao na kwenda sehemu za mbali tangu kulipozuka machafuko katika eneo na Kaskazini mwaka mmoja uliopita. Kujitokeza kwa hali ya sintofahamu kwenye eneo hilo kumewafanya wakulima wengi kuingiwa na wasiwasi wa kurejea nyumbani.