Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban asihi uongozi imara wa Marekani katika kukabiliana na changamoto za kimataifa

Ban asihi uongozi imara wa Marekani katika kukabiliana na changamoto za kimataifa

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon ametoa wito kwa serikali ya Marekani iendelee kuongoza katika kukabiliana na changamoto nyingi za kikanda na za kimataifa, wito ambao ametoa wakati wa ziara yake mjini Washington, ambako amekutana na kufanya mashauriano na Waziri mpya wa Mambo ya nje wa Marekani, John Kerry.

Viongozi hao wawili wamejadili masuala kadhaa, yakiwemo mizozo ya Syria na Mali, pamoja na jaribio la zana za nyuklia lililofanywa na Jamhuri ya Korea Kaskazini wiki hii, ambalo wamelitaja kama uchokozi wa moja kwa moja dhidi ya jamii ya kimataifa.

(SAUTI YA BAN)

 “Uongozi wa Marekani utabaki kuwa muhimu katika siku zijazo. Wakati familia na serikali kote duniani zinahisi mzigo mkubwa kifedha, manufaa ya kushirikiana na Umoja wa Mataifa ni dhahiri- kugawana mzigo, matumizi ya busara ya fedha za umma na kupata masuluhu ya kimataifa. Natazamia  kuimarisha ushirikiano wa Umoja wa Mataifa na Marekani, kwenye njia ya kufikia malengo yetu ya pamoja ya amani, maendeleo na haki za binadamu”

Masuala mengine waliyojadili ni lile la nyuklia Iran, amani ya Mashariki ya Kati, masuala ya maendeleo endelevu, pamoja kuhimiza uungaji mkono wa kampeni ya kupinga dhuluma dhidi ya wanawake ya One Billion Rising.