Chanjo dhidi ya homa ya manjano kuanza Chad: WHO

14 Februari 2013

Wizara ya Afya nchini Chad imepanga kuanza chanjo ya dharura ya jumla dhidi ya homa ya manjano, kufuatia kuthibitishwa kwa visa viwili vya maambukizi ya homa hiyo mnamo Disemba mwaka 2012.

Kampeni hiyo ya chanjo itafanyika katika wilaya tatu zinazopakana na eneo la Darfur nchini Sudan, ambako visa vya homa ya manjano vilikuwa vimeripotiwa awali, na italenga kuwapa chanjo zaidi ya watu milioni moja, wakiwemo wakazi wa kambi za wakimbizi.

Wilaya hizo ni Goz Beida, Guereda and Adré, kulikotoka sampuli za visa hivyo viwili vilivyothibitishwa na maabara ya kikanda ya Shirika la Afya Duniani (WHO) kuhusu homa ya manjano, iliyopo mjini Dakar, Senegal. Kumeripotiwa visa 139 vinavyodhaniwa kuwa vya homa ya manjano, pamoja na vifo 9.