Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Paza sauti kutetea wanawake na watoto wa kike: Bachelet

Paza sauti kutetea wanawake na watoto wa kike: Bachelet

Kataa ukatili wa majumbani, kataa ubakaji na uhalifu wa kingono. Huo ni ujumbe wa hii leo wa Mkuu wa shirika la masuala ya wanawake la Umoja wa Mataifa, UN-WOMEN  Michelle Bachelet inayofanyika duniani kote ili kutokomeza vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake.

Kampeni hiyo ijulikanayo kama One billion rising inadhaminiwa na shirika la V-Day linaloongozwa na Eve Ensler ambapo Bi. Bachelet ametaka kila mwanaume na mwanamke kujitokeza na kuunga mkono kampeni hiyo ya kutetea wanawake na watoto wa kike.

Bi. Bachelet amesema kampeni hiyo inahusisha pia kutokomeza usafirishaji haramu wa wanawake, ukeketaji na ndoa za umri mdogo. Amesema yeye binafsi anashiriki kampeni hiyo ili kuondoa vitendo hivyo dhalili, vinavyosababisha unyanyapaa, aibu na ubaguzi.

Amesema sauti yake ni kwa ajili ya wale wote waliokumbwa na vitendo hivyo na walio hatarini hivyo kila mtu apaze sauti yake kulinda haki ya kibinadamu na kila mwanamke na mtoto wa kike ya kuishi huru bila ukatili wowote.

Katika kampeni hiyo washiriki wanafanya shughuli mbali mbali ikiwemo kucheza muziki na ujumbe maalum wa kukataa vitendo hivyo pamoja na kushiriki makongamano.