Usalama wa chakula na lishe vipewe kipaumbele katika malengo ya maendeleo: FAO

Usalama wa chakula na lishe vipewe kipaumbele katika malengo ya maendeleo: FAO

Mkutano wa wadau mbalimbali wanaojadili kuhusu ajenda ya maendeleo ya kimataifa baada ya mwaka 2015, umetoa wito wa kufanya usalama wa chakula na lishe kuwa nguzo ya juhudi za maendeleo ya siku zijazo. Mkutano huo umetaka dhamira mpya ziwekwe kwa ajili ya jamii nzima ya kimataifa.

Mjadala huo wa siku mbili kuhusu njaa, usalama wa chakula na lishe katika ajenda ya maendeleo baada ya 2015, umesisitiza kuwa usalama wa chakula na lishe ni uti wa mgongo wa nyanja zingine za maendeleo kama vile ajira, elimu, mazingira na afya, na katika kufikia maisha bora ya mwanadamu siku za usoni.

Mkutano huo umewaleta pamoja watu 180, wakiwemo wawakilishi wa serikali, mashirika ya kimataifa, mashirika ya umma na wadau wa Kamati Kuhusu Usalama wa Chakula Duniani (CFS) kutoka sekta za kibinafsi, na ndilo jukwaa la kwanza jumuishi kujadili masuala ya chakula na lishe.

Mjadala huo unaongozwa na Shirika la Chakula na Kilimo (FAO), likishirikiana  na lile la Mpango wa Chakula, (WFP), Mfuko wa Ufadhili wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD), Bioversity International na serikali za Uhispania na Colombia.