Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Radio yaendeleza demokrasia na maendeleo endelevu: UM

Radio yaendeleza demokrasia na maendeleo endelevu: UM

Ikiwa ni zaidi ya miaka mia moja tangu kuanzishwa kwake, Radio imeripotiwa kuendelea kuwa chombo muhimu katika maisha ya kila siku ya mwanadamu ambapo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon amezungumzia nafasi ya chombo hicho katika kuunganisha watu bila kujali mipaka yao.

Akitoa ujumbe wa siku hii, Bwana Ban amesema katika kipindi hicho radio imeleta mabadiliko makubwa kwa kuelimisha, kuburudisha na kuhabarisha.

(SAUTI BAN)

“Tangu kubuniwa kwake zaidi ya miaka 100 iliyopita, radio imechochea tafakuri, imefungua milango ya mabadiliko na kuwa chombo ambacho kwacho taarifa za kuokoa maisha zinapitishwa. Radio inaburudisha, inaelimisha na inahabarisha. Inaendeleza demokrasia na kuimarisha mawazo.”

Naye Mkurugenzi Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni UNESCO, Irina Bokova amesema radio kwa miaka yote hadi sasa Radio imebakia chombo cha kuwasemea wale wasio na pahala pa kusemea na inatoa fursa kwa watu kubadilishana taarifa mbali mbali.

Bi. Bokova amesema pamoja na mabadiliko ya digitali bado nafasi ya radio iko pale pale na inafikia watu wengi kuliko intaneti au televisheni.

(SAUTI BOKOVA)

“Tunaishi katika zama za digitali, lakini radio bado inabakia kichocheo cha kubadili dunia kwa ajili ya amani ya kudumu na maendeleo endelevu.”