Radio yaunganisha watu na maeneo mengine: Ban

13 Februari 2013

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, ametoa ujumbe wake wa siku ya Radio duniani hii leo na kusema ni fursa kwa kila mtu kusherehekea na kutambua uwezo wa redio wa kuunganisha watu wote hata wale walio masafa ya mbali.

Bwana Ban amesema tangu kubuniwa kwake zaidi ya miaka 100 iliyopita, redio imekuwa chombo cha kuchagiza mawazo, kufungua milango ya mabadiliko na njia ya kutoa habari na maelezo ya kuokoa maisha.

Ametolea mfano wa yeye binafsi ambapo amesema wakati akiwa mvulana alikulia kwenye mazingira masikini baada ya vita vya Korea ambapo hawakuwa na simu wala televisheni lakini radio iliwaunganisha na maeneo mengine ya dunia na kumuongezea ufahamu.

(SAUTI YA BAN)

"Redio huburudisha, huelimisha na kufahamisha. Inaendeleza kujieleza kwa njia ya demokrasia na kushawishi mawazo. Kupitia masafa ya shortwave, hadi FM na satellite, redio hukutanisha watu popote walipo. Katika mazingira ya migogoro na nyakati za mizozo, redio ni kiokozi cha jamii zilizopo hatarini. Redio ina thamani kubwa, na gharama ndogo. Kutoka siku ya kwanza, Umoja wa Mataifa imekuwa ikitumia redio kuwafikia watu kote duniani."

Bwana Ban amesema Radio ya Umoja wa Mataifa humulika masuala yote yaliyoko kwenye ajenda ya Umoja wa Mataifa, tokea maendeleo endelevu hadi kuwalinda watoto na kulinda amani na kuzuia migogoro.