Wananchi wakimbia vijiji, wajificha maporini huko Jamhuri ya Afrika ya Kati

12 Februari 2013

Ujumbe wa pamoja wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR na lile la misaada la Mercy Corps uliokwenda huko Bambari na Kaga Bandoro Jamhuri ya Afrika ya Kati umebaini uporaji na kutelekezwa kwa vijiji kadhaa huku wananchi wakiwa wamejificha maporini wakielezea unyanyasaji waliofanyiwa na waasi hao.

Imeelezwa kuwa hii ni mara ya kwanza tangu kati kati  ya mwezi Disemba mwaka jana kwa eneo hilo lililo kilometa 400 Kaskazini Mashariki mwa mji mkuu Bangui kutembelewa tangu waasi wa Seleka wateke miji mikubwa kaskazini mwa nchi hiyo.

Adrian Edwards ni msemaji wa UNHCR.

(SAUTI YA ADRIAN)

“Kiongozi wa kijiji aliripoti kuwa waasi wawili walimchapa viboko wakimshinikiza awaeleze mahali ambako wanakijiji waliokimbia wameficha mali zao. Huko Bambari kwenyewe kumeripotiwa uporaji wa hali ya juu ikiwemo kwenye bohari  yetu. Hali kama hiyo vile vile imeripotiwa huko Kaga Bandoro eneo ambalo tulitembelea wiki chache zilizopita. Kaga Bandoro iko kilometa 400 kaskazini mashariki mwa Bangui. Tunakadiria kuwa hasara ya jumla iliyopatikana kutokana na kuporwa kwa vifaa vya msaada na uharibifu wa maghala yetu huko Kaga Bandoro na Bambari inafikia dola Laki Tatu na Elfu Kumi na Sita.”

UNHCR imesema bado kuna vikwazo kusambaza misada ya kibinadamu huko Jamhuri ya Afrika ya Kati kutokana na ukosefu wa uhakika wa usalama.