UM wasisitiza ushirikiano katika matumizi ya maji

11 Februari 2013

Umoja wa Mataifa umezindua rasmi mwaka wa kimataifa wa ushirikiano katika sekta ya maji, ikiwa ni fursa kwa nchi kushirikiana katika menejimenti ya rasilimali hiyo adhimu kwa amani na maendeleo ya wote.

Katika ujumbe wake Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon amesema mwaka 2013 ni fursa kwa nchi zote kushirikiana kulinda na kutunza vyema rasilimali ya maji ambayo ni muhimu duniani ambayo inaunganisha mataifa wakati wa matumizi..

Asilimia 90 ya wakazi wa dunia wanaishi katika nchi ambazo zinatumia pamoja maji ya maziwa na mito lakini asilimia 60 ya vyanzo 276 vya maji duniani havina mfumo wa kuwezesha matumizi ya pamoja endelevu.

Bwana Ban amesema ongezeko la mahitaji ya maji pamoja na mabadiliko ya tabianchi vinachochea umuhimu wa nchi kushirikiana ili kuhakikisha kila mtu anapata maji safi na salama.

Amesema ushindani unaongezeka kati ya wakulima na wafugaji, sekta ya viwanda na kilimo, na hata mipakani kwa hiyo ni lazima ushirikiano ukawepo ili rasilimali hiyo iwe na manufaa kwa wote kwa wakati huu na kwa wakati ujao.

Naye mwanasayansi kutoka UNESCO, Ana Persic akizungumza mjini New York, Marekani amesema matumizi holela ya maji na udhibiti mbovu wa rasilimali hiyo ni changamoto hivyo ushirikiano ni muhimu katika ngazi zote kwa kuwa maji ni uhai.

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter