UM walaani mwanamke kuchomwa moto kwa tuhuma za uchawi

8 Februari 2013

Kamishna Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Navi Pillay ameelezea masikitiko yake kufuatia ripoti kuwa mwanamke mmoja huko Papua New Guinea mwenye umri wa miaka 20 aliteswa na kuchomwa moto hadi kufa kwa tuhuma za uchawi siku ya Jumatano.

Taarifa zinasema kuwa mwanamke huyo Kepari Leniata alichomwa moto akiwa hai na kundi la watu linalodaiwa kuwa ni jamaa za mtoto wa kiume ambaye mwanamke huyo anatuhumwa kumuua kwa imani za uchawi. Imeelezwa kuwa jitihada za vyombo vya dola kumuokoa mwanamke huyo zilishindikana.

Pillay amesema tukio hilo linaongeza wasiwasi mkubwa juu ya ongezeko la vitendo hivyo nchini Papua New Guinea na ameitaka serikali kuvitokomeza kwa kuwa ni uhalifu na wahusika wafikishwe mbele ya sheria.

Cecily Poully ni msemaji wa ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa

 (SAUTI YA CECILY)