Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tega sikio kwa redio itangazayo amani, maendeleo na haki za binadamu: Ban

Tega sikio kwa redio itangazayo amani, maendeleo na haki za binadamu: Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, amesema kila mmoja anafaa kuadhimisha Siku ya Redio Duniani kwa kusherehekea uwezo wa redio, na kushirikiana kuufanya ulimwengu uzingatie masafa yanayotangaza amani, maendeleo na haki za binadamu kwa wote.

Katika ujumbe wake wa video, Bwana Ban amesema tangu kubuniwa kwake zaidi ya miaka 100 iliyopita, redio imekuwa chombo cha kuchagiza mawazo, kufungua milango ya mabadiliko na njia ya kutoa habari na maelezo ya kuokoa maisha.

“Redio huburudisha, huelimisha na kufahamisha. Inaendeleza kujieleza kwa njia ya demokrasia na kushawishi mawazo. Kupitia masafa ya shortwave, hadi FM na satellite, redio hukutanisha watu popote walipo. Katika mazingira ya migogoro na nyakati za mizozo, redio ni kiokozi cha jamii zilizopo hatarini. Redio ina thamani kubwa, na gharama ndogo. Kutoka siku ya kwanza, Umoja wa Mataifa imekuwa ikitumia redio kuwafikia watu kote duniani.”

Bwana Ban amesema Radio ya Umoja wa Mataifa humulika masuala yote yaliyoko kwenye ajenda ya Umoja wa Mataifa, tokea maendeleo endelevu hadi kuwalinda watoto na kulinda amani na kuzuia migogoro.