Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UM na wadau watangaza ombi la dola milioni 892.6 kuisaidia D.R.C

UM na wadau watangaza ombi la dola milioni 892.6 kuisaidia D.R.C

Mashirika ya Umoja wa Mataifa, wadau katika masuala ya kibinadamu pamoja na serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), leo wametangaza ombi la dola milioni 892.6 kwa ajili ya kufadhili mpango wa kuchukua hatua za kibinadamu mwaka 2013, ili kusaidia mamilioni ya watu ambao wameathiriwa na uhaba wa chakula, migogoro na magonjwa.

Akizungumza wakati wa kutangaza ombi hilo, Mratibu wa masuala ya kibinadamu katika DRC, Moustapha Soumare, amesema chini ya mpango huo, UM na wadau wake watafanya kila wawezalo ili kuwasaidia kukidhi mahitaji yao muhimu.

Mpango huo unaitikia mahitaji yanayoongezeka ya watu milioni 3.9 kote nchini DRC, wakiwemo milioni 2.7 ambao wamelazimika kuhama makwao, zaidi ya nusu yao wakiwa katika mikoa ya mashariki ya Kivu. Mikoa ya Katanga na Maniema pia imeshuhudia watu kuhama makwao.

Takriban watu milioni 6.4 katika DRC kote DRC wanakumbwa na uhaba wa chakula, huku zaidi ya watoto milioni 2 chini ya miaka mitano wakiwa na utapia mlo ulokithiri.