Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UM wafafanua matumizi ya vyombo visivyo na rubani huko DRC

UM wafafanua matumizi ya vyombo visivyo na rubani huko DRC

Mkuu wa operesheni za ulinzi wa amani ndani ya Umoja wa Mataifa Hervé Ladsous ametolea ufafanuzi matumizi ya vyombo vya anga visivyo na rubani ambavyo umoja huo umependekeza vitumike kwenye maeneo hatari huko Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, DRC.

Bwana Ladsous amesema kuwa vyombo hivyo kimsingi ni sawa na kusema ni kamera zinazoruka angani ambazo jukumu kubwa litakuwa ni kufuatilia hali halisi ya usalama mipakani na vitaimarisha shughuli za ulinzi wa amani.

Ladsous amesema taarifa zitakazokusanywa na vyombo hivyo zitakabidhiwa kwa mkuu wa jeshi la kulinda amani la Umoja wa Mataifa nchini humo na zinaweza pia kupatiwa chombo cha kikanda kitakachoundwa na mkutano wa kimataifa wa nchi za maziwa makuu.

“Nitataja kupeleka vyombo vya anga visivyo na rubani kwenye maeneo ya Kivu kwa ajili ya kufuatilia hali halisi, suala ambalo tayari Baraza la Usalama limeruhusu. Na hilo bila shaka litatuwezesha kufahamu hali ilivyo na bila shaka litawaondoa wale wote wenye nia mbaya katika maeneo hayo.”

Kuhusu Mali amesema jukumu la Umoja wa Mataifa litaamuliwa na Baraza la Usalama pindi serikali ya Mali itakapowasilisha ombi rasmi.