Nchi zinazoendelea zakumbwa na gharama kubwa zaidi katika biashara: ESCAP/Benki ya Dunia

6 Februari 2013

Ingawa uchumi wa kimataifa umepata sura ya kujumuisha wote, takwimu mpya zilizoandaliwa na Tume ya Umoja wa Mataifa kuhusu masuala ya kiuchumi na kijamii kwa maeneo ya Asia na Pasifiki, (ESCAP) na Benki ya Dunia, zinaonyesha kuwa nchi zinazoendelea ndizo zinazobeba mzigo mkubwa zaidi wa gharama ya kufanya biashara.

Takwimu hizo zinaonyesha kuwa licha ya nchi hizo kuanza kujumuishwa zaidi katika mfumo wa biashara ya kimataifa, zinaanzia kwenye daraja la juu ambalo halikutani sambamba na uwezo wao, kwani nchi zilizoendelea zinakwenda kwa mwendo wa kasi hata zaidi. Kwa mujibu wa takwimu hizo, teknolojia duni katika nchi zinazoendelea inachangia kwa kiasi kikubwa gharama za juu katika biashara.

Takwimu hizo, ambazo zimekusanywa kwa kipindi cha kati ya 1995 na 2010, zinakusanywa kwa njia bunifu ambayo inakadiria gharama za biashara katika bidhaa za kilimo na bidhaa zinazoundwa viwandani, na hivyo kufungua nafasi mpya kwa watunga sera na watafiti katika masuala ya biashara jumuishi.