Hatari ya watoto wa kike kukeketwa yapungua, Kenya yatajwa kuwa mfano: Ripoti UM

6 Februari 2013

Ripoti mpya ya Umoja wa Mataifa iliyotolewa leo, siku ya kimataifa ya kutokomeza ukeketaji wa wanawake na watoto wa kike, imesema kuwa hatari ya watoto wa kike kukeketwa imepungua ikilinganishwa na ilivyokuwa zamani.

Ripoti hiyo ya mashirika ya Umoja wa mataifa ya UNICEF linalohusika na watoto na UNFPA la idadi watu, imesema katika nchi 29 barani Afrika na Mashariki ya Kati ambako ukeketaji umeshamiri, ni asilimia 36 tu ya watoto wa kike wenye umri wa kati ya miaka 15-19 wamekeketwa, ikilinganishwa na ilivyokuwa kwa asilimia 53 ya wanawake ambao kwa sasa wana umri wa kati ya miaka 45-49.

Kenya imetajwa mfano wa nchi ambako hatari ya watoto wa kike kukeketwa ni ndogo kwa sasa kutokana na elimu dhidi ya kitendo hicho.

Mkurugenzi Mkuu wa UNICEF Anthony Lake amesema elimu hiyo ni muhimu kwani ukeketaji siyo tu ni kosa bali ni kitendo kinachopaswa kutokomezwa ili kusaidia mamilioni ya watoto wa kike na wanawake kuishi maisha yenye afya.