Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban akerwa na hukumu za Mogadishu dhidi ya mwanamke na mwandishi habari

Ban akerwa na hukumu za Mogadishu dhidi ya mwanamke na mwandishi habari

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, ameelezewa kukerwa na hukumu ya kifungo cha mwaka mmoja, ambayo imetolewa mjini Mogadishu, Somalia dhidi ya mwanamke mmoja na mwandishi wa habari. Mwanamke huyo anadaiwa kubakwa na wanaume wenye silaha na ambao walivalia sare za vikosi vya serikali, wakati akiishi katika kambi ya wakimbizi wa ndani.

Umoja wa Mataifa umeelezea kushangazwa kwake mara kwa mara kuhusu ripoti za ukatili wa kingono ulionea katika kambi mjini Mogadishu na maeneo jirani. Ban amesema uhalifu wa aina hiyo hauripotiwi kadri unavyotakiwa kutokana na hofu inayokumba mashuhuda pamoja na unyanyapaa dhidi ya muathirika na kwamba yahitaji ujasiri wa kipekee kufichua vitendo hivyo.

Amesema pamoja na kwamba Somalia inaibuka katika kipindi kigumu cha vurugu kwa kuwa na serikali yenye taasisi wakilishi na serikali mpya ni vyema ikaweka misingi ya kuheshimu haki za binadamu kwa watu wote na uhuru wa kujieleza.

Bwana Ban ametaka serikali ya Somalia kuhakikisha tuhuma zote za ukatili wa kingono zinachunguzwa kwa kina na wahusika wafikishwe mbele ya sheria na zaidi ya yote ni vyema haki ya mwanamke huyo na mwandishi habari ikapatiwa mchakato wa haki wa kimahakama ikiwemo kupatiwa haki ya kukata rufaa.