Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNDP na ILO zataja sababu za vuguvugu katika nchi za kiarabu

UNDP na ILO zataja sababu za vuguvugu katika nchi za kiarabu

Vuguvugu linaloendelea katika nchi za kiarabu limeweka bayana mazingira duni na ukosefu wa haki za kijamii kwenye nchi hizo katika kipindi cha miongo kadhaa ya utekelezaji mbovu wa uchumi huria.

Hiyo ni kwa mujibu wa ripoti ya hivi karibuni zaidi iliyoandaliwa kwa pamoja na shirika la mpango wa maendeleo la Umoja wa Mataifa UNDP na lile la kazi ILO ambapo inasema kasoro kubwa katika ukanda huo wa nchi za kiarabu ni ulinzi duni wa kijamii na ukosefu wa mashauriano ndani ya jamiii.

Ripoti hiyo imesema sera zilizotekelezwa katika miaka ya 1990 hadi 200 ziliwezesha nchi hizo kushughulikia matatizo ya madeni ya mfumuko wa bei na hivyo kuchochea ukuaji wa uchumi na kutoa fursa za ajira.

Hata hivyo imesema ajira hizo zilijikita zaidi kwenye sekta zenye uzalishaji mdogo na serikali hazikuwa makini kubaini athari za kijamii zitokanazo na sera za kiuchumi.

Ripoti hiyo pia inasema wakati hayo yakiendelea, sekta binafsi haikuwa na ushindani wowote duniani kutokana na viwango vidogo vya uwekezaji, taratibu mbovu za udhibiti wa mazingira na kuwepo kwa matukio makubwa ya upendeleo na rushwa.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, ukuaji wa uchumi katika muongo ujao unategemea utawala bora ambao unapaswa kuimarika ili kuvutia vitegauchumi vya hali ya juu na marekebisho ya kimuundo na kitaasisi.