Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Matibabu ya uraibu wa heroin yanapunguza viwango vya UKIMWI Uhispania: WHO

Matibabu ya uraibu wa heroin yanapunguza viwango vya UKIMWI Uhispania: WHO

Ripoti mpya ya Shirika la Afya duniani, WHO, imesema kuwa nchi ya Uhispania imepiga hatua kubwa katika kupunguza maambukizi na viwango vya virusi vya HIV miongoni mwa watu wanaotumia madawa ya kulevya aina ya heroin, kwa kutoa matibabu dhidi ya uraibu.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo ilochapishwa katika jarida la WHO, ufanisi huu umefikiwa kwa kutumia dawa ya methadone kutibu uraibu wa heroin, usambazaji wa sindano safi za kudunga, pamoja na matibabu dhidi ya HIV.

Mnamo miaka ya 1990, viwango vya maambukizi ya HIV miongoni mwa watu wanaotumia dawa haramu za kudunga kama heroin nchini humo viliwahi kufika asilimia 60. Ripoti hiyo inasema ufahamu huu wa uzoefu wa Uhispania unaweza kutumiwa kusaidia nchi nyingine ambazo zina tatizo la uraibu wa dawa za kulevya.