UNESCO yaanza harakati za ukarabati na uhifadhi wa maeneo ya urithi wa kiasili Mali

2 Februari 2013

“Tunataka hatua za haraka za kulinda na kujenga upya maeneo ya kipekee ya urithi wa kiutamaduni nchini Mali”. Hiyo ni kauli ya Mkurugenzi Mkuu wa  Shirika la Umoja wa Matiaifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni, UNESCO, Irina Bokova, aliyoitoa Jumamosi baada ya kuwasili nchini Mali, ikiwa ni sehemu ya harakati za shirika hilo za kusaidia ulinzi na kukarabati maeneo hayo yaliyoharibiwa kutokana na mapigano yaliyoanzia maeneo ya kaskazini.

Bi. Bokova ambaye anatembelea Mali akiwa ameambatana na Rais François Hollande wa Ufaransa, amekaririwa akisema kuwa uhifadhi na ukarabati wa maeneo hayo ya urithi wa kiutamaduni pamoja na nyaraka mbali mbali za kiasili ni hatua muhimu kwa umoja wa kitaifa na maridhiano wakati huu ambapo wananchi wa Mali wanaimarisha misingi ya amani ya nchi yao.

Mkuu huyo wa UNESCO anatarajiwa kuainisha mpango wa utekelezaji wa harakati hizo za ukarabati wa maeneo ya urithi wa kiutamaduni kwa kushirikiana na serikali ya Mali ambapo UNESCO itasaidia ukarabati na uhifadhi.

Atakuwa na mazungumzo na viongozi wa mamlaka mbali mbali kwenye mji mkuu wa Mali, Bamako na mji wa Timbuktu, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya mpango huo.